Taarifa hii inawasilisha matokeo Muhimu ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi (ILFS) uliofanyika Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia mwezi Julai 2020 hadi mwezi Juni 2021. Utafiti huu ulifanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (OCGS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji. Utafiti wa mwaka 2020/21 ni wa sita kati ya tafiti zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo na wadau wengine.

Historia ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi kwa Tanzania Bara ulianza tangu mwaka 1965 ukiwa ni utafiti wa kwanza kufanyika baada ya uhuru.  Utafiti huu ulifuatiwa na tafiti nyingine zilizofanyika mwaka  1990/91, 2000/2001, 2006 na 2014. Lengo la tafiti hizi ilikuwa ni kukusanya viashiria muhimu vya soko la ajira na takwimu nyingine za kijamii na kiuchumi ambazo zinazohitajika katika uundaji wa sera za kukuza ajira na ufuatiliaji wa mienendo ya ajira na ukosefu wa ajira kama inavyobainishwa kwenye dhamira mbalimbali za maendeleo kitaifa, kikanda na kimataifa zikiwemo:- Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano; Dira ya Maendeleo ya Taifa, 2025; Dira ya Maendeleo ya Zanzibar, 2050; Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063; Dira ya Maendeleo ya Afrika ya Mashariki 2050; na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya 2030 ambayo yamejikita kwenye ukuaji endelevu wa uchumi na kazi zenye staha.

Bonyeza hapa kupakua ripoti ya Utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi (pdf)