Menejimenti za Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zimetakiwa kufungua masikio yao kusikiliza hoja za wajumbe wa Mabaraza ya Wafanyakazi na kuzichukua hoja hizo kwa mtazamo chanya kwani wanayozungumza wajumbe katika vikao hivyo si maoni yao binafsi bali ni maoni ya watumishi wanaowawakilisha. Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua kikao cha Nne cha Baraza la Tano la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kinachofanyika mkoani Iringa.

Dkt. Ndumbaro amewataka pia Wajumbe wa Mabaraza ya Wafanyakazi wanapokuwa katika vikao hivyo kujielekeza katika majadiliano yenye tija kwa kuzingatia hali halisi ya nchi na rasilimali zilizopo ili kupata matokeo chanya. Aidha, amesema uchache wa rasilimali isiwe jambo la kurudisha nyuma utendaji kazi serikalini badala yake uchache huo uwe ni fursa kwa watumishi wa umma kutumia rasilimali chache zilizopo kwa umakini na kwa uadilifu mkubwa na kupata matokeo mazuri. Katibu Mkuu alisisitiza watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kitu ambacho Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikikisisitiza tangu kuingia madarakani. 

 

 

Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amewahakikishia watanzania kuwa Ofisi yake itaendelea kufanyakazi kwa bidii ili kuzalisha Takwimu zinazohitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Dkt. Chuwa alieleza kuwa kumekuwepo mahusiano mazuri ya kiutendaji kati ya Menejimenti na Wafanyakazi kupitia TUGHE Tawi kutokana na mashauriano ya mara kwa mara na mawasiliano ya karibu kati ya pande hizo na kuongeza kuwa hali hiyo imesaidia NBS kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa weledi. Kutokana na hali hiyo, NBS imejipambanua kuwa moja kati ya taasisi za serikali zinazotekeleza majukumu yake kikamilifu na kukidhi matarajio ya wananchi kwa kizingatia malengo yaliyowekwa na Serikali.